Inapakia

Ya Hukumu ya Mwisho

Ya Hukumu ya Mwisho

Ya Hukumu ya Mwisho - Sura ya Ungamo la Imani la Westminster
  1. Mungu ameweka siku ambayo atauhukumu ulimwengu kwa haki kwa njia ya Yesu Kristo, ambaye amepewa na Baba mamlaka yote na hukumu. Katika siku hiyo, si malaika waliokengeuka tu watakaohukumiwa, bali pia watu wote walioishi duniani, watasimama mbele ya kiti cha hukumu cha Kristo, kutoa hesabu ya mawazo yao, maneno yao na matendo yao; na kupokea kulingana na waliyoyafanya katika mwili, yawe mema au mabaya.

    • 578. Matendo 17:31.
    • 579. Yohana 5:22,27.
    • 580. 1 Wakorintho 6:3.
    • 2 Petro 2:4.
    • Yuda 1:6.
    • 581. 2 Wakorintho 5:10.
    • Mhubiri 12:14.
    • Warumi 2:16.
    • Warumi 14:10,12.
    • Mathayo 12:36,37.
  2. Kusudi la Mungu kuweka siku hii ni kudhihirisha utukufu wa rehema yake katika wokovu wa milele wa wateule; na wa haki yake katika hukumu ya waliokataliwa, ambao ni waovu na wasiotii. Kwa maana wakati huo wenye haki wataingia katika uzima wa milele, na kupokea utimilifu ule wa furaha na burudiko litakalotoka katika uwepo wa Bwana: bali waovu, wasiomjua Mungu, na wasioitii injili ya Yesu Kristo, watatupwa katika mateso ya milele, na kuadhibiwa kwa maangamizi ya milele mbali na uwepo wa Bwana, na mbali na utukufu wa nguvu zake.

    • 582. Mathayo 25:31-46.
    • Warumi 2:5,6.
    • Warumi 9:22,23.
    • Mathayo 25:21.
    • Matendo 3:19.
    • 2 Wathesalonike 1:7,10.
  3. Kama vile Kristo anavyotaka tuwe na hakika kabisa kwamba kutakuwa na siku ya hukumu, ili kuwazuia watu wote wasitende dhambi, na kwa ajili ya faraja kubwa zaidi ya watauwa katika dhiki zao: vivyo hivyo anataka siku hiyo isijulikane na wanadamu, ili waweze kuutupa mbali usalama wote wa kimwili, na kuwa macho daima, kwa kuwa hawajui ni saa ipi Bwana atakuja; na wawe tayari daima kusema, Njoo, Bwana Yesu, njoo upesi. Amina.

    • 583. 2 Petro 3:11,14.
    • 2 Wakorintho 5:10,11.
    • 584. Mathayo 24:36,42,43,44.
    • Marko 13:35,36,37.
    • Luka 12:35-37.
    • Ufunuo 22:20.